Waziri Jafo ahimiza wazalishaji kuzingatia viwango
V
WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Suleiman Jafo, amewataka wazalishaji nchini kuzingatia viwango katika uzalishaji wa bidhaa kwa kuwa agenda hiyo ni muhimu katika uimarishaji wa uchumi wa nchi.
Waziri Jafo, alitoa kauli hiyo juzi usiku (Novemba 18) jijini Dar es Salaam katika Maadhimisho ya Siku ya Ubora Duniani na utoaji tuzo za kitaifa za ubora kwa washindi wa msimu wa tano 2024.
"Ndugu zangu naomba tufahamu bidhaa zozote zitaweza kushindana kwenye masoko endapo zitazingatia ubora na hili niishukuru sana TBS (Shirika la Viwango Tanzania), Mkurugenzi na timu yako, mmekuwa watu wa kuzingatia ubora na hii inadhihirisha kwamba hata Barani Afrika taasisi yetu ya TBS ndiyo imekuwa mshindi wa taasisi za ubora," alisema Jafo na kuongeza;
"Kwa hiyo kinachofanywa hapa na TBS ni jambo ambalo taasisi hii barani Afrika inatambulika kwamba ni mshindi namba moja wa taasisi za mambo ya udhibiti wa ubora, niwashukuru sana."
Aidha, alishukuru kampuni na taasisi mbalimbali ambazo zimeendelea kushindana, kwani ushindani huo maana yake ni kujiuza.
Alipongeza taasisi na kampuni ambazo mwaka jana zilishinda na kushika nafasi ya pili na kwamba hiyo inadhihirisha kampuni na taasisi zinazopitishwa na TBS sio wasindikizaji.
"Hiyo ina maana kuwa ni taasisi ambazo zimefanya vizuri nchini mwetu na zina sifa." Alisisitiza Jafo. Aliwaambia wazalishaji kwamba Tanzania ina fursa kubwa, ina masoko mbalimbali, idadi ya watu ni zaidi ya milioni 62 maana yake walaji wa bidhaa zetu wapo,
"Lakini sio hivyo sisi tumepata fursa kubwa , kwa sababu nchi yetu ipo kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) maana yake bidhaa zetu zinapokuwa na ubora zinapata fursa ya kwenda kushinda na kuuzwa katika maeneo mengine katika nchi hizo, ina maana tunapozingatia ubora bidhaa zetu zinakuwa shindani."
Aliongeza kwamba na kwenye mashindano hayo taasisi na kampuni zinapata fursa ya kufahamu kuwa bidhaa zenu zinapata fursa ya kwenda kushindana katika masoko ya Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
"Lakini sio hivyo, kampuni zetu za uzalishaji wa bidhaa zinapata fursa ya kushindana katika soko huru la Afrika , hii ina maana kuwa endapo bidhaa zetu zinazozalishwa zitakuwa shindani zitapata fursa ya masoko katika maeneo mbalimbali," alisema Jofo na kuongeza;
"Lakini sio hilo tu hata masoko mengine tutakayopata katika nchi nyingine za mbali, kwa mfano soko la Ulaya, India, China na kwingine.
Kwa hiyo kinachofanywa na TBS kinatupa fursa ni kusaidia kampuni zetu ziweze kupandisha viwango vya ubora na kuweza kupata masoko katika maeneo mbalimbali.
Aidha, Waziri Jafo aliipongeza TBS akisema mikutano mbalimbali ambayo ameshiriki ikiwemo wa hivi karibuni nchini Ethiopia, Tanzania inatajwa vizuri kwa baadhi ya bidhaa zetu zinazoenda nje ya nchi zinakidhi ubora wa viwango.
"Maana yake TBS mmefanya wajibu wenu nawahakikishieni jambo hilo linaenda vizuri, lakini niwaombe wazalishaji, tuhakikishe uzalishaji wetu wa bidhaa unazingatia viwango, kwa kufanya hivyo maana yake mnatendea haki Taifa letu, jambo la pili tunatendea haki walaji, lakini hilo litaweza kuleta thamani kwa bidhaa zetu zinazokwenda nje.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa TBS, Ashura Katunzi, alisema Maadhimisho haya ya Siku ya Ubora Duniani hufanyika kila mwaka yakienda sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Ubora ambayo huadhimishwa kila mwaka katika wiki ya pili ya mwezi Novemba.
Alisema TBS imeadhimisha Wiki hii ya Ubora kwa kutoa elimu kwa wananchi kuhusiana na masuala ya ubora katika vyombo mbalimbali vya habari ili kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi zitakazowasaidia kuelewa masuala ya ubora kwa ujumla na kufanya maamuzi sahihi.
Alisema Kauli mbiu ya mwaka huu inasema; “From Compliance to Performance” yaani Kutoka kwenye uzingatiaji wa viwango hadi utendaji ambayo inatufundisha kuwa si tu kwamba inahitajika kuzingatia viwango vya ubora, bali pia kuhakikisha kwamba tunatekeleza viwango hivyo kwa vitendo katika kila kipengele cha maisha yetu na shughuli zetu.
Alisema wanatambua na kuthamini hatua mbalimbali zinazoendelea kuchukuliwa na nchi chini ya usimamizi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayosimamiwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kujenga sekta ya, viwanda na biashara yenye ushindani hapa nchini.
"Hatua hizi zinatarajiwa kuwezesha bidhaa na huduma zetu kushindana kote ulimwenguni, hasa wakati huu ambao huduma na bidhaa kutoka kwenye nchi nyingine zinaruhusiwa kuuzwa hapa nchini," alisema Dkt. Katunzi na kuongeza;
Katika zama hizi tulizopo ni ngumu kuzuia bidhaa na huduma kutoka kwenye nchi moja kuuzwa kwenye nchi nyingine kutokana na uwepo wa kanuni za kimataifa hususani kanuni za WTO zinazozuia kuweka vikwazo vya kiufundi kwenye biashara yaani WTO Technical Barrier to Trade Agreement. Kwa sababu hiyo njia bora ya kulinda soko la bidhaa na huduma zetu ndani na nje ya mipaka yetu ni kuzalisha bidhaa na kutoa huduma zenye ubora wa hali ya juu na kwa gharama nafuu.
Wazalishaji na watoa huduma wanahitajika kujengewa au kujijengea utamaduni wa ubora na ushindani hapa nchini. Vilevile wanahitaji kufahamu uhusiano kati ya ubora na ushindani. Hii ndiyo njia pekee kwa nchi yetu kusonga mbele kibiashara, hasa katika Mapinduzi ya Nne ya Viwanda.