Historia
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ni taasisi ya Viwango ya Taifa la Tanzania iliyoanzishwa na Serikali kama sehemu ya jitihada ya kuimarisha miundombinu kwa sekta za viwanda na biashara kwenye uchumi nchini. Shirika hili lilianzishwa kwa sheria ya Bunge Na.3 ya Mwaka 1975 kama Taasisi ya Viwango ya Taifa na kuanza rasmi kazi tarehe 16 Aprili, 1976. Baadaye ilibadilishwa jina na kuwa Shirika la Viwango Tanzania kwa Sheria Na.1 ya mwaka 1977. Tarehe 20 Machi 2009, Sheria ya Viwango Na. 3 ya mwaka 1975 ilitanguliwa na kubadilishwa na Sheria ya Viwango Na. 2 ya mwaka 2009.
Shirika hili limeanzishwa kama sehemu ya jitihada za Serikali ili kuimarisha miundombinu saidizi ya kitaasisi kwa sekta za viwanda na biashara za uchumi. TBS hasa imepewa mamlaka na wajibu wa kuchukua hatua na kudhibiti ubora wa bidhaa za aina mbalimbali na kuhimiza uzingatiaji viwango katika viwanda na biashara.
Kazi na wajibu
Kwa mujibu wa kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Viwango Sura 130 TBS ina kazi kuu zifuatazo:
a) Kuchukua hatua za kudhibiti ubora wa bidhaa, huduma na mazingira ya aina mbalimbali na kuhimiza uzingatiaji wa viwango katika viwanda na biashara.
b) Kuweka utaratibu au kuwezesha upimaji wa bidhaa na ugezi wa vifaa kwa usahihi na wakati kwa kutambua kiwango cha usahihi na ufuatiliaji kwa kulinganisha na viwango vilivyoidhinishwa na Waziri wa Viwanda na Biashara kwa mapendekezo ya Bodi ya Wakurugenzi na kutoa hati kuhusiana navyo.
c) Kuweka utaratibu au kuwezesha uchunguzi na upimaji wa bidhaa na kitu kingine chochote ambacho kitazalishwa, kuchakatwa au kusindikwa.
d) Kuthibitisha usajili na udhibiti wa matumizi ya alama za ubora kwa mujibu wa masharti ya Sheria ya Viwango.
e) Kutoa, kuongeza muda, kusitisha, kubadili au kufuta leseni yoyote iliyotolewa kwa ajili ya kutumia alama yoyote ya ubora.
f) Kuvisaidia viwanda katika kuweka na kuhimiza uhakiki wa ubora na taratibu za mifumo ya usimamizi wa mazingira.
g) Kuandaa, kubadili au kurekebisha viwango vya kitaifa.
h) Kutoa elimu kuhusiana na uwekaji viwango, udhibiti ubora, ugezi, upimaji na mazingira.
i) Kuisaidia Serikali au mtu mwingine yeyote katika uandaaji wa viwango.
j) Kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali, wawakilishi wa viwanda au mamlaka nyingine au mtu kwa lengo la kuwezesha matumizi sahihi ya viwango.
k) Kuwezesha ukaguzi, uchukuaji wa sampuli na kupima bidhaa zilizotengenezwa nchini na zinazoagizwa kutoka nje ya nchi kwa lengo la kubaini kama bidhaa hizo zinatimiza masharti ya Sheria ya Viwango au sheria nyingine yoyote inayoshughulikia viwango vinavyohusiana na bidhaa hizo.
l) Kukagua na kusajili majengo ya bidhaa za chakula na vipodozi kwa mujibu wa sheria.
m) Kuthibitisha na kusajili bidhaa za vyakula na vipodozi kwa mujibu wa sheria.
n) Kuwa msimamizi wa viwango vya vipimo vya kitaifa kwa kurekebisha, kubadili au kufuta viwango vyovyote pale itakapoonekana kuwa marekebisho, ubadilishaji au ufutaji huo ni muhimu katika kudumisha utimizaji wa viwango vya kimataifa.
o) Kuwa mtia saini wa utaratibu wa utambuzi wa pamoja na taasisi nyingine za vipimo vya kitaifa.
p) Kukusanya, kuchapisha na kusambaza machapisho na nyenzo nyingine kuhusu uwekaji wa viwango vinavyokubaliwa, mambo mengine yanayohusiana nayo na kutoa nyenzo zitakazowawezesha wananchi kupata vifaa hivyo.
q) Kufanya, kuhimiza na kusaidia utafiti kuhusu uwekaji viwango vinavyokubaliwa na mambo mengine yanayohusiana na masuala ya viwango na udhibiti ubora.
r) Kushiriki au kuandaa mikutano, warsha, semina na majadiliano kwa mambo yanayohusu shughuli za TBS.
s) Kushirikiana na mashirika ya kikanda na ya Kimataifa kwa mambo yote yanayohusiana na uandaaji wa viwango na uhakiki wa ubora na kuiwakilisha nchi kwenye mambo hayo.
t) Kuchapisha kila baada ya muda toleo jipya la viwango vya taifa kwa ajili ya wingi/ kiasi na vipimo vitakavyotumika kulingana na toleo jipya la mfumo wa kimataifa wa vipimo.
u) Kufanya uhakiki wa utekelezaji wa matakwa ya viwango kabla ya usafirishaji wa bidhaa husika (PVoC).
v) Kuchukua hatua zote nyingine na kufanya shughuli zozote ambazo zitaonekana na Bodi ya Wakurugenzi kuwa na manufaa au umuhimu kwa utendaji bora na wenye ufanisi wa TBS.
Katika utendaji wa kazi zake TBS inajali zaidi afya, usalama, mazingira na ustawi wa jamii wa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kutumia kadri iwezekanavyo, mfumo wa mawasiliano na ushirikiano na taasisi yoyote iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria yoyote ya nchi na kazi zinazofanana au zinazohusiana na viwango vya viwanda au biashara kwa ujumla.