TBS yatunukiwa Cheti cha Umahiri na WCO
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limepata cheti cha utambuzi na umahiri kutoka Shirika la Forodha Duniani ( WCO) kwa kutambua mchango wake katika jumuiya ya umoja wa forodha duniani, hususani katika kuwezesha biashara na kulinda afya ya jamii.
Cheti hicho kimetolewa Januari 26,2026 na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, kwa niaba ya WCO, kwa Mkurungezi wa TBS, Ashura Katunzi katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Forodha kwa mwaka 2026
Akizungumza baada ya kupokea cheti hicho, Mkurugenzi wa TBS, Dkt Ashura Katunzi amesema shirika hilo lina wajibu mkubwa wa kulinda usalama na ubora wa bidhaa zinazoingia nchini ili kuwalinda Watanzania dhidi ya bidhaa hafifu au hatarishi, sambamba na kuwezesha biashara halali zinazofanyika katika sekta ya viwanda.
Amesema Cheti hicho ni alama ya kutambua mchango na kazi kubwa ambayo TBS imekuwa ikiifanya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, huku akisisitiza kuwa mafanikio hayo yametokana na mazingira wezeshi yanayoendelea kuwekwa na Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara.
“Cheti hiki ni uthibitisho wa dhamira yetu katika kulinda afya ya jamii kupitia uangalizi na uwajibikaji, pamoja na mchango wetu katika kurahisisha biashara na kukuza sekta ya viwanda,” amesema Dkt Katunzi
Aidha, TBS imetoa rai kwa Watanzania kufanya biashara katika mazingira wezeshi yaliyopo.
Pia imehaidi kuendelea kutoa uwezeshaji katika sekta ya viwanda na biashara, pamoja na kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa bora na salama wakati wote.