Naibu Waziri Londo ajivunia uwekezaji wa Serikali TBS
Serikali imesema uwekezaji unaofanywa katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS) umeongeza uwezo wa taasisi hiyo kulinda afya za Watanzania, thamani ya fedha za wananchi na kusaidia bidhaa zinazozalishwa nchini kushindana katika masoko ya ndani na kimataifa.
Hayo yesemwa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, alipofanya ziara yake TBS, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujifunza na kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Shirika hilo, ambapo pia alijionea shughuli zinazofanyika kwenye maabara.
Londo alisema TBS ni mshirika muhimu wa Serikali katika kuhakikisha bidhaa zinazotumiwa na wananchi zinakidhi viwango vya ubora na usalama, huku wazalishaji wakisaidiwa kuboresha bidhaa zao na kupata fursa ya kufikia masoko mapana zaidi.
Alisema ziara hiyo imempa fursa ya kuzungumza na watumishi wa TBS na kujionea namna taasisi hiyo inavyotekeleza majukumu yake kwa kutumia mashine na vifaa vya kisasa ilivyowezeshwa na Serikali.
“Taasisi hii ni muhimu kulinda afya ya Watanzania, lakini pia kuangalia thamani ya fedha ya Mtanzania kulingana na matumizi ya bidhaa anazotumia inalindwa. Kwa hiyo, kimsingi TBS ni mshirika muhimu ndani ya Wizara ya Viwanda na Biashara,” alisema.
Katika hatua nyingine, Londo amewataka wazalishaji na wajasiriamali kutumia huduma zinazothibitishwa na TBS bila hofu.
Alisisitiza kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha kupata huduma za viwango kwa urahisi.
Alisema baadhi ya wazalishaji wamekuwa na hofu ya kufuata taratibu za kupata alama ya ubora ya TBS kutokana na kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mchakato huo, wakihofia kuwa unaweza kuwa mrefu au kuwa na gharama kubwa.
Alisema Serikali kupitia TBS imeendelea kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Saluhu Hassan ya kuhakikisha taasisi hiyo inawafikia wananchi na kuwasaidia, hususan wajasiriamali wadogo, vijana na wanawake.
“Tunataka kuhakikisha TBS inawafikia Watanzania na inawasaidia Watanzania, hasa wale wa hali ya chini. Tumeona kwa mifano TBS ikiwafikia wajasiriamali vijana na akina mama, ikiwapa mafunzo, lakini pia kuthibitishwa bidhaa bure kwa gharana za Serikali,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, alisema uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika maabara za taasisi hiyo umeongeza uwezo wake wa kuhakikisha ubora na usalama wa bidhaa zinazotumiwa na Watanzania.
Katunzi alosema baadhi ya maabara zimewekewa mashine na vifaa vya kisasa vyenye thamani ya mabilioni ya fedha, hali ambayo imeongeza uwezo wa TBS kufanya vipimo mbalimbali kwa ufanisi na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini na zinazoingizwa zinakidhi viwango vinavyotakiwa.
“Ndani ya maabara zetu tuna uwekezaji mkubwa ambao waandishi wa habari mmeuona katika maabara mbalimbali. Kwa mfano, katika maabara hii ya uchambuzi wa chakula, kuna uwekezaji usiopungua Sh bilioni tano, huku mashine mbalimbali zikifikia takribani Sh bilioni 10 kwenye eneo moja,” alisema.
Alisema uwekezaji huo una umuhimu mkubwa katika kulinda afya na usalama wa Watanzania kwa kuhakikisha bidhaa zinazofika sokoni zina ubora unaokubalika na hazijachakachuliwa.
Alisema TBS itaendelea kumlinda mtumiaji wa bidhaa nchini huku ikiwawezesha wazalishaji na wafanyabiashara wa Tanzania kuzalisha bidhaa zenye viwango vinavyoweza kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.