SHIRIKA LA VIWANGO TANZANIA(TBS)
e-Services

Bodi ya Wakurugenzi TBS yatembelea mipaka ya Tunduma na Kasumulu

Reason Image

BODI ya Wakurugenzi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ikiongozwa na Mwenyekiti wake Prof. Othman Chande Othman imefanya ziara ya kutembelea ofisi za TBS zilizopo katika mipaka ya Tunduma na Kasumulu ili kujionea shughuli zinazofanyika.

Dhumuni la ziara hiyo ni kuona changamoto zilizopo na kuzitafutia mkakati na kuielekeza Menejimenti ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao na kuwezesha biashara.

Aidha Bodi hiyo imefanya ziara hiyo Desemba 10 katika mpaka wa Tunduma mkoani Songwe na Desemba 11 kwenye mpaka wa Kasumulu mkoani Mbeya.

Pamoja na hayo ,Bodi imeielekeza menejimenti ya TBS kuja na mikakati ya bidhaa zinazoingia kupitia njia za panya na kukwepa ukaguzi ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu ya madhara ya kutumia bidhaa ambazo hazijathibitishwa ubora wake na TBS.

Aidha, Bodi imeagiza menejimenti hiyo kuja na mkakati wa kuhakikisha bidhaa zilizokaguliwa kutoka nje na zinazozalishwa nchini kuwa na alama maalum ambayo itamwezesha mlaji wa mwisho kujua bidhaa anayotaka kununua iwapo imekaguliwa na TBS.

Maelekezo hayo yametolewa na Bodi hiyo kufuatia Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, kuieleza kuwa bidhaa ambazo hazijakaguliwa na Shirika hilo vikiwemo vipodozi vilivyopivwa marufuku, zimeendelea kuwepo kwenye soko kutokana na uwepo wa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kutumia njia zisizo rasmi kuingiza bidhaa hivyo.

Alisema kwenye njia zote rasmi za kuingizia bidhaa ikiwemo mipakani, viwanja vya ndege na bandarini, TBS ina wakaguzi wanaoshirikiana na mamlaka nyingine za udhibiti, lakini changamoto ni bidhaa hizo kuingizwa nchini kwa njia za panya.

Hapo ndipo Bodi ikasema hiyo inaonesha uhitaji wa bidhaa hizo ni mkubwa nchini, ikahimiza Shirika kuendea kutoa elimu kwa wananchi pamoja na kuziwekea alama maalum bidhaa zilizokaguliwa ili wananchi wazitambue Kwa urahisi.



Settings